Friday, November 2, 2007

MAPINDUZI KATIKA TIMU YA SIMBA

ENYEKITI wa zamani wa muda aliyewahi kuiongoza timu ya Simba ya jijini Dar es Salaam, Michael Wambura na kiongozi wa kundi la Friends of Simba Evance Aveva, wanatarajiwa kuiongoza klabu hiyo katika mapinduzi yanayotarajiwa kufanyika Jumapili.

Habari za uhakika zilizopatikana ndani ya klabu zinasema kwamba mkutano wa dharula ambao unamlenga Mwenyekiti wa klabu hiyo Hassan Dalali ‘Field Marshal’ anatarajiwa kupinduliwa na nafasi yake kuchukuliwa na Wambura au Aveva kwa madai ya timu kufanya vibaya.

Mtoa habari huyo anasema kwamba baada ya kuona timu inaendelea kufanya vibaya katika Ligi ya Vodacom inayoendelea katika viwanja mbalimbali, Dalali ameshtuka na kupinga mkutano kwa nguvu zote .

Mkutano huo uliotangazwa hivi karibuni na Kaimu Katibu Mkuu wa Simba Said Rubeya ‘Seydou’ kuitisha mkutano wa Wanachama kujadili mwenendo mbaya wa timu yao katika Ligi Kuu.

Akizungumzia kuhusu mkutano huo Dalali, alisema kuwa mkutano ni batili kikatiba kwa sababu wanachama tayari walishafanya mikutano miwili yaani wa Aprili na Agosti, hivyo mkutano uliobaki utafanyika Desemba ili kuzungumzia mapato na matumizi.

Dalali alisema kuwa haogopi mapinduzi kwani katika maisha yake hajali kabisa mambo hayo.

Wakati hali ikiwa hivyo, baadhi ya Wanachama wa Simba jana walifika kwenye ofisi za Sayari na kusema kuwa wanaunga mkono kauli ya Seydou kufanya mkutano Jumapili unaotarajiwa kufanyika makao makuu ya klabu hiyo.

Wanachama hao Khamis Ng’ombo mwenye kadi 0113, Fatuma Mohammed 1880, Zintanga Maji 3305 na Mashaka Ally 0770, kwa pamoja walisema kuwa Wanachama wajitokeze kwa wingi kwenye mkutano huo utakaoanza saa 4:00 asubuhi.

Akizungumza kwa niaba ya wanachama Ng’ombo alisema kuwa mkutano huo utazungumzia matatizo baina ya timu kufanya vibaya kwani waliwatembelea wachezaji kambini waliwaambia kuwa uwezo wanao lakini wanamatatizo na viongozi wao.

Alisema kuwa viongozi hawawatimizii mahitaji muhimu , hivyo tunaomba siku hiyo wanachama wajitokeze kwa wingi kujadili masuala mbalimbali ya klabu ikiwamo mikataba ya wachezaji inaisha mwezi huu.

“Sisi wanachama matatizo ya klabu yanatakiwa kujadiliwa na viongozi na wanachama ili kuinusuru klabu pamoja na timu hivyo kisheria tunayohaki ya kuitisha mkutano huo ambao tunashukuru Seydou ameona mbali na kuamua kuitisha mkutano,” alisema Ng’ombo.

Alisema kuwa wakati waliwatembelea wachezaji ilikuwa ni kabla ya mechi na watani wao Yanga waliwaahidi kuwa watashinda lakini walisema wana matatizo kitendo ambacho walikifanya kwani waliishinda Yanga bao 1-0.

Ng’ombo alisema kuwa timu yao wanaamini iko imara hivyo wamesisitiza wanachama kufika kwa wingi ili kuweza kuinusuru klabu hiyo wasisikilize maneno ya Dalali kwani yeye ni Msimamizi tu , mtendaji ni katibu ambaye katiba inamruhusu kuitisha mkutano.

Mwisho .

No comments: