Wednesday, February 3, 2010

Ada ya mtihani ipo palepale

Wizara yawaambia wazazi walipe haraka

*msamaha utaanza baada ya bajeti 2010/11

Na mwandishi wetu

MATUMAINI ya wanafunzi wa shule za Sekondari kulipiwa ada ya mtihani na serikali kwa mwaka huu yametoweka baada ya wizara ya Elimu na mafunzo ya ufundi kubainisha kwamba mpango huo utaanza rasmi Mwaka kesho.

Akizungumza na Tanzania Daima jijini Dar es Salaam, Jana Afisa habari wa wizara hiyo Magdalena Kishiwa alisema kuwa wanafunzi wa Mwaka huu wanapaswa kulipa ada ya mtihani kama kawaida.

Kishiwa alisema kuwa ingawa serikali imefuta ada hiyo baada ya kubaini kuwa wanafunzi wengi wanashindwa kufanya mtihani kwa kukosa pesa ,lakini mpango huo utaanza kutekelezeka baada ya Mwaka wa Pesa unaonza julai.

“ni kweli tayari hata sisi tumepokea malalamiko wazazi wakigoma kulipia watoto wao ada kwa madai kuwa serikali imefuta ada ,lakini wajue kuwa Mwaka pesa unaanza julai,kwa hiyo hata hizo pesandipo zitatengwa”alisema Kishiwa

Alisema kuwa wanafunzi watakaochelewa kulipa ada hiyo wakitegemea Serikali watakumbana na faini au kuzuiliwa matokeo yao kwa mjibu wa taratibu za Baraza la mtihani (NECTA).

Afisa habari huyo ameliambia Tanzania Daima kuwa baadhi ya wananchi waliposikia taarifa hiyo walifikiri inaanza mara moja akutekelezwa bila kujua kuwa lazima kwanza itengwe bajeti ya kuwalipia.
Hivi karibuni Waziri wa Elimu na ufundi, Profesa Jumanne Magembe, alitangaza kufuta ada ya mitihani kwa wanafunzi wanaosoma shule za sekondari zinazomilikiwa na serikali tu.
Taarifa hiyo ilitolewa siku chache tu baada ya serikali kueleza sababu za kuendelea kushuka kiwango cha ufaulu nchini.
Pia aliziagiza shule zote za sekondari nchini kutumia mfumo wa kitabu kimoja cha kufundishia, utakaowasaidia watungaji mitihani kuwa na mawazo ya pamoja.
.
“Hii ni changamoto nyingine iliyojitokeza katika majadiliano yetu, takwimu hapa zinaonyesha kuwa zaidi ya wanafunzi 30,000 walitarajia kufanya mtihani wa kidato cha pili lakini walishindwa kutokana na kukosa ada ya mtihani,” alisaema Profesa Maghembe.

Alisema kwa wanafunzi wa kidato cha pili, serikali itatenga bajeti ya gharama za uchapaji mitihani hiyo kupitia ofisi ya mkaguzi mkuu wa shule, ambapo watahiniwa wa vidato vya nne na sita serikali italiwezesha Baraza la Mitihani la Taifa.