Friday, January 29, 2010

ni marufuku mfanyakazi kupokea asante.


Singita Grumeti Reserves;Hoteli inayowapora wafanyakazi jasho lao


Na Mwandishi wetu

TANGU serikali imefungua milango ya uwekezaji hapa nchini Miaka michache iliyopita na kuruhusu wageni kuingia nchini kuwekeza bado haijaweka mazingira mazuri yanayowajali wazawa.
badala yake mazingira yaliyopo kwasasa yanaonekana kuwajali zaidi wawekezaji hivyo wananchi wazalendo ambao wangefurahia kupata ajira kutoka kwa wawekezaji wamegeuka watumwa na vibarua.
uchunguzi uliofanywa na Tanzania Daima kwa muda mrefu umebaini kuwa wawekezaji wengi wa kigeni wanapowasili hapa nchini hujenga mahusiano ya karibu kwa viongozi wa Serikali na vyama vya wafanyakazi ili kulinda masilahi yao.
Hali hiyo huwafanya wafanyakazi wengi wanaobahatika kupata ajira katika makampuni ya kigeni kukosa sehemu ya kulalamikia hata kama wananyanyaswa na wawekezaji hao.
miongoni mwa maeneo ambayo yameonekana kulalamikiwa na wafanyakazi ni kwenye makampuni ya madini nay ale yanayoendesha Kambi za kulala watalii na mahoteli makubwa .
Kampuni ya Singita Game Reserves kutoka Afrika kusini ambayo inaendesha biashara ya watalii na Hoteli katika mbunga ya Taifa Serengeti baada ya kuingia ubia na kampuni ya Grumet Game Reserve ni miongoni mwa makampuni yanayolalamikiwa.
kutoka na ubia huo ndipo ikaundwa kampuni inayoendesha biashara hiyo inayojulikana kama Singita Grumeti Reserves ambayo inamiliki hoteli maarufu ya Singita Lodge ambayo ina sehemu tatu ambazo ni Sasakwa Lodge, Sabora Tented Camp na Faru Faru Lodge zote zipo Serengeti.
hotel hizi ambazo zina hadhi ya nyota tano ndio zinatajwa kuwa ghali kabisa hapa nchini kuliko hotel nyingine kwani kwa siku moja mteja hulipa kati ya Dolla 1600 hadi 1800 wakati Hotel Maarufu kama Kilimanjaro Hotel Kempinski bei ya kulala kwa siku moja ni Dolla 240.
hali hiyo huwafanya watalii wanaotembelea hoteli hiyo kuwa ni wale matajiri wakubwa ambao hufika katika Hotel hiyo kwa ajili ya kuangalia wanyama na kupiga picha.
hata hivyo katika mazingira kama hayo ambayo wafanyakazi wazalendo walitegemea kupata maisha bora badala yake wameangukia katika dhuluma inayowafanya wasichukue zawadi wanazopewa na ‘matajiri’ hao.
wafanyakazi hao ambao wamepata nafasi ya kuzungumza na Tanzania Daima wamesema kuwa utawala wa hoteli hiyo kutoka Afrika kusini umekuwa ukiwanyanyasa kwa kuchukua ‘asante yao’ yaani tip kama inavyofahamika ambayo hupewa na wageni hao.
ili kutimiza malengo yao ,wawekezaji hao wameweka matangazo katika sehemu mbali mbali za hoteli hiyo wakiwaonya wageni wasiwape zawadi yoyote wafanyakazi wao badala yake waikabidhi kwao, ili wao ndio wawape wafanyakazi.
“kama unaavyojua Hoteli yetu inapokea wageni ambao ni matajiri wakubwa kwa hiyo ukimhudumia vizuri mgeni anaweza kukupatia hadi dola 500 anapotaka kuondoka lakini makaburu wanaoendesha hoteli hiyo wanazichukua zote”anasema mfanyakazi wa kitengo cha usafi wa vyumba ‘hausekeeping’
baada ya pesa hizo kuingia mikononi mwa viongozi wa Hoteli hiyo inadaiwa kuwa ndio hutumika kulipia kodi ya pango serikalini kitu ambacho wafanyakazi wanaona ni kunyanyaswa kwasababu hilo ni jasho lao.
“tunaitaka Serikali ichunguze mapato ya hoteli hii, tunawasiwasi huenda hizi tip zetu ndio hutumika kulipa kodi serikalini halafu kile kinachozalishwa hapa kianpelekwa chote nje kama faida”anasema mmoja wa wafanyakazi hao.
wakati wafanyakazi hao wakitoa malalamiko hayo , Meneja mwajiri wa Hoteli hiyo Nelson Mafie anatetea hatua hiyo kwa madai kuwa wanazikusanya pesa zote kisha wanazigawanya sawa kwa wafanyakazi wote hata wale ambao wasingemfikia mgeni kiurahisi.
“Hili ni suala la ndani umelipataje wewe? kwanza tip sio kitu cha lazima wala wageni hatuwalazimishi kutoa tip ni suala lenye kujitolea tu..na wala sio sehemu ya mishahara ambayo wanapaswa kulalamikia”anasema Mafie
Mafie anasema kuwa wafanyakazi hao hawana haki ya kulalamika kwasababu wanaendelea kupokea mshahara wao kama kawaida na hoteli ya Singita inawafanyakazi 620 hivyo zile pesa zinakusanywa kisha zinagawanywa kwa wote lakini baada ya kukatwa kodi ya Serikali.
“kwanza huo sio mshahara hadi walalamike, sisi tunawafanyakazi zaidi ya 620 sasa huyo anayetaka pesa anatamaa kwasababu pesa hizo kama mtalii ametoa Dolla moja kwanza tunakata kodi ya serikali inayobaki tunawagawia sawa”anasema Mafie.
madai hayo yanapingwa na wafanyakazi hao kugawiwa pesa sawa kwa maelezo kwamba hakuna chombo maalumu kinachodhibitisha kiasi cha pesa kinachokuwa kimetolewa na wageni hao ili wanapogawiwa hesabu iwe sawa.
“ndugu Mwandishi kama tulivyokuambia pale wageni wanaokuja sio wale wenye njaa, kama kwa siku moja analipa Dolla 1800 kulala tu siku anaondoka kukuachia dola 1000 sio tatizo kwake,lakini uliza utakachopata
mara nyingi uongozi wa Hoteli yetu unawaambia wageni hao kuwa nchi hii ni masikini hivyo wale wageni kwa huruma yao hutoa zawadi mbalimbali lakini utakuja kuambulia shilingi 50,000 baada ya miezi sita, wakati kila siku wageni wanaingia na kutoka katika Hoteli zetu ”anasema Dada mmoja Mkazi wa Kijiji cha Nyichoka.
licha ya gharama kuwa kubwa katika hoteli hiyo lakini idadi ya wageni wanaofika hapo ni kubwa jambo ambalo linafanya mgeni anayetaka kwenda hapo kutoa miezi mitatu kabla ili kuachiwa nafasi hali inayodhibitisha kwamba wageni wanapishana hapo.
mfanyakazi mwingine ambaye amekuwa akifanya kazi ya kuhudumia vinywaji katika hoteli hiyo anasema kuwa amekuwa na bahati ya kupewa zawadi mbalimbali kama simu na kamera lakini hajawahi kuzipokea hata moja.
‘kutokana na matangazo kukataza tusipokee zawadi hizo moja kwa moja mtalii anaweza kukuambia kuwa nimekupa hii kamera lakini naipeleka mapokezi wakupatie ,anawaleza kabisa kuwa kamera hii ni ya fulani lakini anapoondoka hutaiona tena hiyo Kamera”anasema mfanyakazi huyo.
Tanzania Daima ilipowasiliana na Mwenyekiti wa chama cha wafanyakazi wa hifadhi za taifa , mahoteli na majumbani, (CHODAWU) tawi la Serengeti Magesa Wambura kama anayafahamu malalamiko hayo ambapo aliyakana.
“haya wanayoyasema inawezekana yapo au hayapo lakini hao wafanyakazi walipaswa kuandika malalamiko yaende kwenye menejimenti ...najua kwamba matatizo yapo lakini walipaswa kufuata taratibu zote kwa kupitia ngazi husika kuliko kupeleka kwenye vyombo vya habari”anasema Magesa
mwenyekiti huyo ambaye pia ni Kaimu Mwenyekiti wa Mkoa wa Mara anasema kuwa hajawahi kusikia malalamiko hayo wala kuyapiokea lakini alimtaka mwandishi awasiline na uongozi wa Hoteli hiyo.
wafanyakazi hao wanapoulizwa kama wamewahi kuwasilisha malalamiko yao kwenye chama chao, wanasema kuwa suala kama hilo wanaogopa kufanya hivyo kwani ni kama kujifukuzisha kazi wenyewe kutokana na uhusiano uliopo kati ya viongozi wa chama chao na Hoteli.
katika uchunguzi mwingine unaonyesha kuwa baadhi ya viongozi wa CHODAWU katika tawi hilo wanatuhumiwa na wanachama wao kutokana na mahusiano ya karibu waliojenga na menejimenti ya Singita baada ya kupewa tenda ya kuwasambazia vitu.
naye Kaimu Katibu Mkuu wa CHODAWU taifa Kiwanga Towele akizungumzia malalamiko hayo ,anasema kuwa suala la tip ni haki ya mfanyakazi na lipo kila mahali katika hoteli kubwa.
Towele ambaye amefanyakazi katika hoteli zaidi ya Miaka 17 anasema kuwa ingawa katika mahoteli mengine wanakusanya kwanza zawadi zawadi au pesa hizo lakini wanachombo au mfuko kamili unaoratibu kiasi cha pesa kinachoingia ili kuweka mahesabu sawa.
“Tena katika hoteli nyingi za ulaya suala la tip limekuwa kama sheria badala ya utamaduni, unakuta wamekuandikia katika zile taratibu zao kwamba baada ya kuondoka ni lazima utoe tip kama asante kwa ajili ya kuongeza morali kwa wafanyakazi”anasema Towele
Katibu huyo anasema kuwa katika Hoteli hiyo kulikuwa na kero nyingi ambazo wafanyakazi walikuwa wakizilalamikiwa kutokana na manyanyaso yanayotolewa na makaburu lakini walijitahidi Disemba Mwaka jana wakakaa wakayamaliza ingawa suala hilo halikuwemo kwenye ajenda.
break.news@yahoo.com




























·




No comments: